Ijumaa, 18 Agosti 2017

KWANINI WATANZANIA WENGI SI WAHAIDHINA?

Tanzania Conservatives     Agosti 18, 2017     No comments

Utangulizi

Kutokana na hali ya kisiasa inavyoendelea siku hadi siku inaonekana ni wazi kuwa demokrasia haiwi kwa mfumo ambao ni chanya kwa taifa kwa ujumla. Najua wazi kuwa utashangaa na kujiuliza swali, “huyu ndugu haoni kuwa demokrasia imekuwa kwa kiasi kikubwa hivi, anafikiri nini?”. Ndio kwa macho ya kawaida mtu anaweza kusema kuwa demokrasia imekuwa kwa kiasi kikubwa kama vile ambavyo wanasiasa baadhi wanahubiri kwenye majukwaa yao kila siku. Kwangu mimi naona bado kabisa demokrasia haijawa, ndio tunaanza kujifunza jinsi ya kutumia mfumo huo kwa manufaa ya taifa. Kuna mitazamo miwili hapa; mosi ni demokrasia ndani ya chama na pili ni demokrasia kwa ujumla wa kitaifa. Nikizungumzia demokrasia ndani ya chama naanza kugusia pia mrengo wa chama husika katika siasa za dunia hii. Vyama vingi havielezi kwa undani juu ya imani yao na mrengo wao wa kisiasa wanaoufuata. Hili ndio linazaa hoja yangu na swali ambalo ndio kichwa cha habari cha hoja hiyo, “kwa nini Watanzania wengi si wahafidhina?” utasikia katika vijiwe na mitaani watu wanavyolalamika kuonewa na kudhulumiwa, utaona viongozi kukosa  nidhamu kwa wananchi, kuwa wababe, wasioambilika wala kusikia lolote la mtu mdogo. Sasa kwanza nigusie juu ya imani au itikadi ya wahafidhina (Consevatives) wengi duniani hasa katika mkondo wa kisiasa wa mrengo wa kulia (right wing):
  • Nguvu ya Umma. Ukisoma na kufanya rejea za IDU (International Democratic Union) na vyama ambavyo viko kwenye umoja huo wanaamini katika nguvu ya umma (people’s power). Siasa zao mara nyingi ni za harakati na wana sera ambazo zina jikita katika kuwapa wananchi nguvu ya kufanya maamuzi. Ukiagalia nchi mfano Ghana ambapo chama kinachoongoza sasa (2017) kimo katika umoja huo.
  • Kuchaguliwa na kulinda demokrasia. Wanaamini katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi unaoweka chama madarakani kwa kufuata uchaguzi wa vyama vingi. Vyama vya mfumo na mrengo wa kulia wanaamini katika chaguzi za haki ambazo zinaweka utawala wa wananchi madarakani.
  • Fikra na mamlaka ya umma ndio inayotumika kupinga unyanyasaji na kutetea jamii. Kulinda na kuthamini fikra za umma ndio hutumika kupinga unyanyasaji kutokana na hii hapa ndipo ambapo mrengo wa kulia unakuwa na uhafidhina. Mfano nchini Marekani wakati ambapo aliyekuwa rais wa kipindi hicho Ndg. Ibrahim Lincolin, aliweza kusaini hati ya kuwafanya Wamarekani weusi kuwa huru dhidi ya utumwa. Pia Repulican walipitisha haki kwa Negroes kupiga kura na haki ya kusoma bila upendeleo.
  • kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutumia raslimali za nchi. Katika zama za sasa nchi haiwezi kukua kama wananchi wake hawajakuwa kimapato. Mfano mapato mengi ya taifa hutegemea kodi inayokusanywa kutoka kwa wananchi; kama kipato cha wananchi ni kidogo ni ngumu sana kwa serikali kupata kipato ambacho ni kizuri kwa ustawi wa maendeleo. Pato litashuka kwa kiwango kikubwa sana.
  • Kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huru, utakaoheshimu na kulinda haki na mali za watu, biashara huru na sekta ya watu binafsi.  Ili kukuza soko la bidhaa katika taifa ni vyema kukuza na kuimarisha soko huria soko lenye ushindani kwa mujibu wa taratibu na maono ya kibiashara. Ushindani katika soko hujenga jamii yenye kushindana katika ubunifu na uboreshaji kwa lengo la kupata wateja wengi.
  • Matumizi bora ya raslimali asilia za nchi ili zichangie kikamilifu katika pato la taifa. Matumizi bora ya rasilimali za  taifa husaidia sana katika kukuza mapato ya taifa kwa wananchi. Hii ni kutokana na miraaba ambayo itakuwa ya tija kwa asilimia nzuri. Unaweza kuona kuwa katika hili tumepwaya sana na kinaitajika chama ambacho kina mrengo wa kihafidhina kurejesha hili.
  • Uzalendo na kuthamini mila na desturi za taifa. Ukiangalia katika siasa za ulimwengu, vyama ambavyo vina mrengo huu mara nyingi huwa na itikadi ya kujenga taifa kwanza paasipo kuegemea kwenye utandawazi kwa kiwango kikubwa; utaifa kwanza kwa maneno mengine. Uzalendo kwa watu wenye mrengo huu ni mkubwa sana kulinganisha na watu wenye mrengo wa shoto ambao wameegemea katika siasa za utandawazi zaidi, ambazo kwa kiasi kikubwa zinaweza kupora mali za umma na kupeleka kwa watu wa mataifa kwa jina la wawekezaji. Nieleweke vizuri hapa kwamba uwekezaji si dhambi hata wahafidhina wanataka wawekezaji katika uchumi wao ila uwekezaji huo uwe wa tija zaidi; taifa linufaike vyema kwa hilo.

Hitimisho

Kuna mengi mazuri juu ya mrengo wa kati kulia na kulia kwa umoja wake. Ni moja kati ya mrengo ambao unajali na kuthamini uhuru na demokrasia ya watu. Swali la kwanini Watanzania wengi sio wahafidhina linaweza kujibiwa kwa kutokana na historia ya siasa za hapa nchini tangu wakati wa uhuru. Wale wote ambao walionekana kuwa na nguvu katika siasa na waliokuwa wafuasi na walimu wa mrengo huo waliuliwa nguvu na kupewa sifa mbaya katika jamii. Jamii ilidanganywa na kuyumbishwa juu ya ukweli wa elimu ya siasa. Kufutwa kwa masomo ya siasa na kutokuwepo kwa mtaala thabiti wa kutoa elimu hiyo ilitolewa na kizazi kikubwa hakijapata elimu hiyo. Hata baadhi ya wanasiasa nguli na maarufu hawajui misimamo yao katika mrengo na ndio maana ni wepesi wa kupelekwa huku na huko. Wananchi wanahitaji kuelimishwa.

0 maoni :

Popular Post

Subscribe to Newsletter

We'll never share your Email address.
© 2015 Tanzania Conservative. Designed by Conservative. Powered by Blogger.